Wednesday, January 20, 2010

SOMO LA QUR'AN TUKUFU:Suratul An'aam Aya ya 4 - 9

Katika darsa hii tutazungumzia aya sita za sura hiyo, tukianza na aya ya nne na ya tano ambazo zinasema:
Na haiwafikii hata ishara moja katika ishara za mola wao Mlezi ila wao huwa wenye kuikengeuka.Wameikanusha haki ilipowajia. Basi zitawajia khabari za yale waliyokuwa wakiyakejeli.
Katika aya tatu za mwanzo za sura hii ambazo tulizisoma katika darsa yetu iliyopita, Mwenyezi Mungu Mola wetu Mlezi alitutajia baadhi ya ishara zake, ambazo ni za uumbaji wa mbingu, ardhi na mwanadamu; na vile vile akatukumbusha juu ya umri ulio na mpaka na ule wa mwisho tunaoupitisha katika maisha yetu ya hapa duniani. Aya tulizosoma hivi punde zinasema, baadhi ya watu, pamoja na kuzishuhudia ishara hizo na nyinginezo za Allah katika ulimwengu waishio, wanaamua kuikadhibisha haki badala ya kuiamini na kuifuata. Kwa maneno mengine ni kuwa, baadhi ya watu, sio kwamba hawazioni ishara za kuwatambulisha haki bali ukweli ni kuwa, hawana nia ya kuikubali hiyo haki. Sawa kabisa na mtu aliyejifanya amelala, ambaye mbali ya kumwamsha kwa sauti, hata kama utampigia tarumbeta pia katu hatofumbua jicho lake, bali ataendelea kujifanya amelala. Hali ya kuwa mtu aliyelala kweli kama utamwamsha kwa kutumia njia moja au nyingie, bila shaka yoyote mwishowe ataamka tu. Lakini aya ya tano ya suratul An-aam inawataka watu wenye sifa ya aina hiyo wajue kwamba, mwenendo wao huo una mwisho wake, nao ni siku watakapoipata jaza ya amali na matendo yao, wakati ambapo hata kama watagutuka toka kwenye usingizi wao huo wa kimaonyesho watakuwa wamechelewa, kwani maji yatakuwa yamekwishamwagika na hivyo hayatozoleka tena. Kutokana na aya hizi tunajielimisha kwamba, kwa mtu mkaidi na mfanya inadi ambaye nia yake si kutaka kuijua haki, hakuna hoja, ishara au ushahidi wa aina yoyote ule wa kumtambulisha haki atakaoukubali. Kwa hakika mtu wa aina hiyo ni sikio la kufa ambalo kamwe halisikii dawa. Tunaindeleza darsa yetu kwa aya ya sita ambayo inasema:
Je huoni uma ngapi tulizoziangamiza kabla yao? Tuliwamakinisha katika nchi tusivyokumakinisheni nyinyi, na tukawapelekea mvua nyingi wakastarehe kwa kila namna na mazo, na tukaifanya mito inapita mbele yao. Kisha tukawaangamiza kwa sababu ya dhambi zao, na tukaumba baada yao, uma nyingine.
Aya hii inawahutubu watu wanaoipinga haki kwa sababu ya ukaidi na inadi tu na kusema kuwa, hivi nyinyi hamujaipitia historia ya kaumu zilizotangulia? Kwani nyinyi hamujapata khabari za watu wa tamaduni na uma zilizopita, ambazo zilikuwako kabla yenu na ambazo ziliangamizwa? Je mnadhani nyinyi mna nguvu zaidi na suhula za ziada kuwashinda wao, kiasi cha kuhisi na kudhani kwamba, mtaweza kutoka nje ya milki na mamlaka ya Mwenyezi Mungu? Basi sivyo hivyo, kwani baadhi ya kaumu zilizopita zilikuwa na nguvu na suhula kushinda nyinyi, lakini kwa kuwa walizitumia vibaya neema tulizowateremshia kwa kuzifanyia mambo maovu na kumuasi Mola wao, tuliwaangamiza na kuwaleta badala yao watu wa kaumu nyingine. Naam, hivyo ndivyo ilivyo, ni kwamba, mbali ya mtu mmoja mmoja kuhesabiwa na kulipwa jaza ya matendo yake mema na mabaya aliyoyatenda yeye binafsi, jamii za wanaadamu kwa ujumla pia, kila moja ina hatima na jaala yake, ambayo ni matokeo ya amali na matendo yafanywayo na wengi wa watu wa jamii hizo. Kwa mantiki hiyo basi tunajifunza kutokana na aya hii kuwa, kuisoma historia na kupata ibra na mazingatio kutokana na hatima ya kaumu zilizopita ni njia mojawapo ya kujielimisha mtu, ambayo imeusiwa sana na Quran na viongozi wa dini. Funzo jingine tunalolipata hapa ni kuwa, matukio na mabadiliko yanayojiri katika historia, ni natija ya matendo yanayofanywa na watu waishio katika zama mbalimbali za historia ya mwanaadamu, na huo ni utaratibu aliouweka mwenyewe Allah (sw) katika maisha ya wanaadamu wa kuziangamiza jamii zilizotopea kwenye maovu na maasi. Waaidha tunajielimisha kuwa suhula za kimaada, si kipimo hasa au siri ya kupatia saada na fanaka, kwani wangapi na wangapi miongoni mwa watu ambao kwa sababu ya kughurika na kujisahau kwa neema hizo za kimaada, wamekuwa sababu na chanzo cha kuangamizwa wao wenyewe, na jamii zao kwa ujumla? Tunaendelea na darsa yetu kwa kuipitia aya ya saba ambayo inasema:

Na lau tungelikuteremshia maandishi katika karatasi kama walivyotaka, na wakayagusa maandishi hayo kwa mikono yao, bila shaka wale waliokufuru wangelisema, haya si chochote ila ni uchawi dhahiri.
Kama historia inavyonukuu, ni kwamba Washirikina wa Kikureishi waliokuweko Makka walimwendea Bwana Mtume Muhammad (saw) na kumwambia kuwa, sisi tutakuwa tayari kuamini kama utateremsha maneno ya Mungu yakiwa yameandikwa kwenye karatasi kama ambavyo Mwenyezi Mungu aliiteremsha Taurati kwa Musa ikiwa imeandikwa juu ya jiwe, na hivyo Musa kuwapelekea watu wake mbao za taurati kutoka Turi. Jibu la Quran kwa Washirikina hao ni kuwa, hata kama wangelifanyiwa hilo pia, basi wangelisema: ‘Huu ni uchawi tu, wala si muujiza wa Mwenyezi Mungu', kama ambavyo wengi miongoni mwa watu wa Nabii Musa waliozishuhudia kwa macho yao mbao za Taurati hawakumuamini Nabii huyo, na badala yake wakamwita kuwa ni mchawi. Tunaihitimisha darsa hii kwa aya ya nane na ya tisa ambazo zinasema :
Na husema mbona hakuteremshwa Malaika wa kutwambia kuwa kweli huyu ni Mtume. Na kama tungeliteremsha Malaika na juu ya hivi wakakataa, bila shaka shauri yao ya kuangamizwa ingekatwa mara moja, kisha wasingepewa muhula. Na kama Mtume tungelimfanya Malaika, bila shaka tungelimfanya kwa sura za binadamu naye tungelimvisha kile wanachovaa wao.
Moja ya visingizio vingine vilivyokuwa vikitolewa na makafiri wa Kikureishi kama sharti la kuwa tayari kusilimu na kumuamini Nabii Muhammad (saw), ni kutaka kumuona Malaika wa wahyi kwa macho yao au kuwa Malaika huyo Mtume mwenyewe anayewalingania Waislamu. Quran tukufu imevijibu visingizo hivyo kwa kusema :' kama mnataka mumuone malaika, naye pia itabidi tukuteremshieni akiwa katika umbo la mwanadamu, ambapo bado itakuwa ni mushkili kwenu kuweza kumtambua kuwa ni malaika, na hivyo kama angeteremshwa mngesema huyu naye ni mtu kama sisi. Isitoshe ni kuwa, kama mngeliweza kumtambua kuwa ni malaika basi mngelazimika kumuamini na wala kusingepatikana upenyo wowote wa kuikwepa haki. Hali ya kuwa, kwa mwenendo wa ukaidi na inadi mlionao, tuna hakika kuwa msingelikubali haki, ambapo katika hali hiyo kusingekuwepo na shauri jingine ghairi ya kuteremshiwa adhabu na kuangamizwa nyote. Kwa hivyo jueni basi kwamba kutokubaliwa ombi lenu hilo na Mwenyezi Mungu kumetokana na rehma na upole wake kwenu. Kwa hakika aya hizi zinaonyesha kwa uwazi kabisa jinsi tabia chafu za ghururi na kiburi zilivyowafanya baadhi ya wanaadamu wasiwe tayari kamwe kumtii binaadamu aliye sawa na wao, na hivyo kuukana utume wake. Watu hao walikuwa wakidhani kwamba Mtume wa Mungu ilipasa awe ni kiumbe malaika, na aliye katika daraja ya juu kuliko wanaadamu, ilhali Nabii anayetumwa kwa watu hawi mfikishaji wahyi tu bali yeye pia huwa ni kigezo cha maneno na matendo kwa binaadamu wenzake, na kwa hiyo haiyumkiniki malaika kuwa kigezo cha kufuatwa na wanaadamu katika maisha yao, mwanadamu ambaye hisia, matashi na ghariza zake za kimaumbile zinatafautiana kabisa na kiumbe malaika. Kutokana na aya hii tunajielimisha kuwa, kama mtu atakuwa mtafutaji haki, basi ushahidi na muujiza mdogo kabisa unatosha kuziamsha hisia zake za kimaumbile na kifitra kwa ajili ya kuikubali haki hiyo; lakini kama atakuwa mkaidi na mtafuta visingizio, hata akiteremkiwa na malaika kutoka mbinguni, bado ataendelea kuikana na kuikataa kata kata haki.

No comments:

Post a Comment