Wednesday, January 20, 2010

SOMO LA QUR'AN TUKUFU:Suratul An'aam Aya ya 4 - 9

Katika darsa hii tutazungumzia aya sita za sura hiyo, tukianza na aya ya nne na ya tano ambazo zinasema:
Na haiwafikii hata ishara moja katika ishara za mola wao Mlezi ila wao huwa wenye kuikengeuka.Wameikanusha haki ilipowajia. Basi zitawajia khabari za yale waliyokuwa wakiyakejeli.
Katika aya tatu za mwanzo za sura hii ambazo tulizisoma katika darsa yetu iliyopita, Mwenyezi Mungu Mola wetu Mlezi alitutajia baadhi ya ishara zake, ambazo ni za uumbaji wa mbingu, ardhi na mwanadamu; na vile vile akatukumbusha juu ya umri ulio na mpaka na ule wa mwisho tunaoupitisha katika maisha yetu ya hapa duniani. Aya tulizosoma hivi punde zinasema, baadhi ya watu, pamoja na kuzishuhudia ishara hizo na nyinginezo za Allah katika ulimwengu waishio, wanaamua kuikadhibisha haki badala ya kuiamini na kuifuata. Kwa maneno mengine ni kuwa, baadhi ya watu, sio kwamba hawazioni ishara za kuwatambulisha haki bali ukweli ni kuwa, hawana nia ya kuikubali hiyo haki. Sawa kabisa na mtu aliyejifanya amelala, ambaye mbali ya kumwamsha kwa sauti, hata kama utampigia tarumbeta pia katu hatofumbua jicho lake, bali ataendelea kujifanya amelala. Hali ya kuwa mtu aliyelala kweli kama utamwamsha kwa kutumia njia moja au nyingie, bila shaka yoyote mwishowe ataamka tu. Lakini aya ya tano ya suratul An-aam inawataka watu wenye sifa ya aina hiyo wajue kwamba, mwenendo wao huo una mwisho wake, nao ni siku watakapoipata jaza ya amali na matendo yao, wakati ambapo hata kama watagutuka toka kwenye usingizi wao huo wa kimaonyesho watakuwa wamechelewa, kwani maji yatakuwa yamekwishamwagika na hivyo hayatozoleka tena. Kutokana na aya hizi tunajielimisha kwamba, kwa mtu mkaidi na mfanya inadi ambaye nia yake si kutaka kuijua haki, hakuna hoja, ishara au ushahidi wa aina yoyote ule wa kumtambulisha haki atakaoukubali. Kwa hakika mtu wa aina hiyo ni sikio la kufa ambalo kamwe halisikii dawa. Tunaindeleza darsa yetu kwa aya ya sita ambayo inasema:
Je huoni uma ngapi tulizoziangamiza kabla yao? Tuliwamakinisha katika nchi tusivyokumakinisheni nyinyi, na tukawapelekea mvua nyingi wakastarehe kwa kila namna na mazo, na tukaifanya mito inapita mbele yao. Kisha tukawaangamiza kwa sababu ya dhambi zao, na tukaumba baada yao, uma nyingine.
Aya hii inawahutubu watu wanaoipinga haki kwa sababu ya ukaidi na inadi tu na kusema kuwa, hivi nyinyi hamujaipitia historia ya kaumu zilizotangulia? Kwani nyinyi hamujapata khabari za watu wa tamaduni na uma zilizopita, ambazo zilikuwako kabla yenu na ambazo ziliangamizwa? Je mnadhani nyinyi mna nguvu zaidi na suhula za ziada kuwashinda wao, kiasi cha kuhisi na kudhani kwamba, mtaweza kutoka nje ya milki na mamlaka ya Mwenyezi Mungu? Basi sivyo hivyo, kwani baadhi ya kaumu zilizopita zilikuwa na nguvu na suhula kushinda nyinyi, lakini kwa kuwa walizitumia vibaya neema tulizowateremshia kwa kuzifanyia mambo maovu na kumuasi Mola wao, tuliwaangamiza na kuwaleta badala yao watu wa kaumu nyingine. Naam, hivyo ndivyo ilivyo, ni kwamba, mbali ya mtu mmoja mmoja kuhesabiwa na kulipwa jaza ya matendo yake mema na mabaya aliyoyatenda yeye binafsi, jamii za wanaadamu kwa ujumla pia, kila moja ina hatima na jaala yake, ambayo ni matokeo ya amali na matendo yafanywayo na wengi wa watu wa jamii hizo. Kwa mantiki hiyo basi tunajifunza kutokana na aya hii kuwa, kuisoma historia na kupata ibra na mazingatio kutokana na hatima ya kaumu zilizopita ni njia mojawapo ya kujielimisha mtu, ambayo imeusiwa sana na Quran na viongozi wa dini. Funzo jingine tunalolipata hapa ni kuwa, matukio na mabadiliko yanayojiri katika historia, ni natija ya matendo yanayofanywa na watu waishio katika zama mbalimbali za historia ya mwanaadamu, na huo ni utaratibu aliouweka mwenyewe Allah (sw) katika maisha ya wanaadamu wa kuziangamiza jamii zilizotopea kwenye maovu na maasi. Waaidha tunajielimisha kuwa suhula za kimaada, si kipimo hasa au siri ya kupatia saada na fanaka, kwani wangapi na wangapi miongoni mwa watu ambao kwa sababu ya kughurika na kujisahau kwa neema hizo za kimaada, wamekuwa sababu na chanzo cha kuangamizwa wao wenyewe, na jamii zao kwa ujumla? Tunaendelea na darsa yetu kwa kuipitia aya ya saba ambayo inasema:

Na lau tungelikuteremshia maandishi katika karatasi kama walivyotaka, na wakayagusa maandishi hayo kwa mikono yao, bila shaka wale waliokufuru wangelisema, haya si chochote ila ni uchawi dhahiri.
Kama historia inavyonukuu, ni kwamba Washirikina wa Kikureishi waliokuweko Makka walimwendea Bwana Mtume Muhammad (saw) na kumwambia kuwa, sisi tutakuwa tayari kuamini kama utateremsha maneno ya Mungu yakiwa yameandikwa kwenye karatasi kama ambavyo Mwenyezi Mungu aliiteremsha Taurati kwa Musa ikiwa imeandikwa juu ya jiwe, na hivyo Musa kuwapelekea watu wake mbao za taurati kutoka Turi. Jibu la Quran kwa Washirikina hao ni kuwa, hata kama wangelifanyiwa hilo pia, basi wangelisema: ‘Huu ni uchawi tu, wala si muujiza wa Mwenyezi Mungu', kama ambavyo wengi miongoni mwa watu wa Nabii Musa waliozishuhudia kwa macho yao mbao za Taurati hawakumuamini Nabii huyo, na badala yake wakamwita kuwa ni mchawi. Tunaihitimisha darsa hii kwa aya ya nane na ya tisa ambazo zinasema :
Na husema mbona hakuteremshwa Malaika wa kutwambia kuwa kweli huyu ni Mtume. Na kama tungeliteremsha Malaika na juu ya hivi wakakataa, bila shaka shauri yao ya kuangamizwa ingekatwa mara moja, kisha wasingepewa muhula. Na kama Mtume tungelimfanya Malaika, bila shaka tungelimfanya kwa sura za binadamu naye tungelimvisha kile wanachovaa wao.
Moja ya visingizio vingine vilivyokuwa vikitolewa na makafiri wa Kikureishi kama sharti la kuwa tayari kusilimu na kumuamini Nabii Muhammad (saw), ni kutaka kumuona Malaika wa wahyi kwa macho yao au kuwa Malaika huyo Mtume mwenyewe anayewalingania Waislamu. Quran tukufu imevijibu visingizo hivyo kwa kusema :' kama mnataka mumuone malaika, naye pia itabidi tukuteremshieni akiwa katika umbo la mwanadamu, ambapo bado itakuwa ni mushkili kwenu kuweza kumtambua kuwa ni malaika, na hivyo kama angeteremshwa mngesema huyu naye ni mtu kama sisi. Isitoshe ni kuwa, kama mngeliweza kumtambua kuwa ni malaika basi mngelazimika kumuamini na wala kusingepatikana upenyo wowote wa kuikwepa haki. Hali ya kuwa, kwa mwenendo wa ukaidi na inadi mlionao, tuna hakika kuwa msingelikubali haki, ambapo katika hali hiyo kusingekuwepo na shauri jingine ghairi ya kuteremshiwa adhabu na kuangamizwa nyote. Kwa hivyo jueni basi kwamba kutokubaliwa ombi lenu hilo na Mwenyezi Mungu kumetokana na rehma na upole wake kwenu. Kwa hakika aya hizi zinaonyesha kwa uwazi kabisa jinsi tabia chafu za ghururi na kiburi zilivyowafanya baadhi ya wanaadamu wasiwe tayari kamwe kumtii binaadamu aliye sawa na wao, na hivyo kuukana utume wake. Watu hao walikuwa wakidhani kwamba Mtume wa Mungu ilipasa awe ni kiumbe malaika, na aliye katika daraja ya juu kuliko wanaadamu, ilhali Nabii anayetumwa kwa watu hawi mfikishaji wahyi tu bali yeye pia huwa ni kigezo cha maneno na matendo kwa binaadamu wenzake, na kwa hiyo haiyumkiniki malaika kuwa kigezo cha kufuatwa na wanaadamu katika maisha yao, mwanadamu ambaye hisia, matashi na ghariza zake za kimaumbile zinatafautiana kabisa na kiumbe malaika. Kutokana na aya hii tunajielimisha kuwa, kama mtu atakuwa mtafutaji haki, basi ushahidi na muujiza mdogo kabisa unatosha kuziamsha hisia zake za kimaumbile na kifitra kwa ajili ya kuikubali haki hiyo; lakini kama atakuwa mkaidi na mtafuta visingizio, hata akiteremkiwa na malaika kutoka mbinguni, bado ataendelea kuikana na kuikataa kata kata haki.

Suratul An'aam Aya ya 1 - 3

Sura hii iliteremshwa Makka na ina aya 165. Ujumbe mkuu wa sura hii ni kupamabana na shiriki na kulingania tauhidi kumpwekesha Mwenyezi Mungu); na hivyo nyingi kati ya aya zake zinabainisha itikadi za uzushi za Washirikina na Waabudu masanamu na kuweka wazi ubatilifu wa itikadi hizo. Aya za sura hii ya sita ya Quran Tukufu zinazungumzia pia masuala ya halali na haramu ya wanyama wa aina mbalimbali. Kwani kutokana na imani potofu walizokuwa nazo, Washirikina wa Kikureishi walijiharamishia baadhi ya wanyama ambao waliwaitakidi kwamba haijuzu kula nyama zao wala kuwatumia kama vipando. Ni kwa sababu ya kuzungumzia hukumu mbali mabali za wanyama wa miguu minne, ndiyo maana sura hii imepewa jina hili la al An-aam. Baada ya utangulizai huu mfupi, kwa pamoja sasa na tuitazame aya ya kwanza ya sura hii inayosema:
Sifa zote ni za Mwenyezi Mungu aliyeumba mbingu na ardhi na akafanya giza na mwangaza. Tena baada ya haya wale waliokufuru wamewafanya wengine sawa na Mola wao.
Aya hii tukufu inaanza kwa kumtambulisha Allah (sw) kwa waja wake na hasa wale wanaomshirikisha na pia wanaokanusha moja kwa moja kuwepo kwake. Aya inamtaja Mwenyezi Mungu kuwa ni yule aliyeumba mbingu na ardhi, hivyo kuwataka waeleze wale wanaoabudu asiyekuwa yeye, je hicho wanachokiabudu wao, kinao uwezo nacho wa kuumba? Aya inaendelea kusema , Mola huyo Allah, kwa kulipa nuru na mwangaza jua ameufanya ulimwengu yaani dunia hii ineemeke kwa mwangaza wenye joto unalohitajia, na kwa kuweka utaratibu maalum wa kuzunguka sayari mbali mbali, akalileta na giza kwa ajili ya mapumziko ya viumbe; sasa hao miungu wenu manowaabudu wanazo nguvu na uwezo wa kufanya kama hayo? Hapana shaka yeyote majibu ya masuali mawili hayo ni ‘hapana'. Kwa hivyo basi muelekeeni na kumuabudu Mola aliye mmoja na mweza wa kila kitu, na mhimidini na kumsifu Mola huyo kwa kuumba ulimwengu kama huu kwa ajili yenu. Aya hii inatoa maelezao ambayo yanavunja hoja za wanaoamini maada yaani Materialists amabo wanakana kabisa kuwepo muumbaji wa Ulimwengu huu, aidha inawarudi Washirikina yaani wanaoabudu Mungu zaidi ya mmoja, kama walivyo wafuasi wa dini ya Zartosht ambao itikadi yao ni kuwa mwangaza na giza ndiyo vyanzo vya ulimwengu. Kadhalika inavunja imani na itikadai potofu ya Washirikina wanaomuitakidi Allah kuwa ni Mungu aliye na mshirika. Kuna nukta moja yenye kutoa mguso wa kuvutia hapa, nayo ni namna Quran inavyoitaja nuru katika hali ya umoja tu, wakati neno giza daima linaonekana ndani ya kitabu hicho kitukufu katika sura ya wingi; hii ikimaanisha kwamba kwa kuwa nuru au mwangaza ni dhihirisho la uongofu, na kwa vile uongofu au haki ni moja tu, hivyo neno ‘muangaza' limekuja katika hali ya umoja. Lakini kwa vile njia za batili na upotofu ni nyingi, hivyo, kiza ambacho ni kielelezo chake kimekuja katika sura ya wingi. Kutokana na aya hii tunajielimisha kuwa Allah (sw) ndiye muumbaji wa kila kitu, na kwa hakika kuwepo au kutoweka kwa kila kitu kunafungamana na yeye. Tunajifunza pia kwamba, shirki ni aina mojawapo ya kufru. Kwani kukiitakidi kitu cho chote kile kuwa ni mshirika wa Allah, maana yake ni kukataa uwezo mutlaki wa Mola Muumba wa kukiendesha peke yake kila kitu cha ulimwengu huu.
Aya ya pili ya sura hii inasema:
Yeye ndiye aliyekuumbeni kwa udongo, kisha akakuwekeeni ajali, na muda maalumu uko kwake tu. Tena baada ya haya nyinyi mnafanya shaka.
Katika aya iliyopita , imezungumziwa kudura na uwezo mutlaqi wa Allah (sw) wa kuumba mbingu na ardhi. Katika aya hii linazungumziwa suala la kuumbwa mwanadamu kutokana na udongo usio na uhai, na kuhoji kuwa kama uhai na mauti yenu nyote yako mikononi mwa Mwenyezi Mungu, inakuwaje mnatilia shaka kuwepo kwake ? Katika aya hii zimetajwa ajali au nyakati mbili katika uhai wa mwanadamu , moja ikiwa ni muda wa ajali maalumu ambao anaujua Allah peke yake, na mwingine ni muda usio maalumu ambao unategemea mazingira ya kimaisha ya kia mtu. Kimsingi ni kwamba, Mwenyezi Mungu amemruzuku kila mtu uwezo na kipaji maalumu, uwezo ambao unapomalizika uhai wa mtu pia huisha, sawa na taa inayozimika baada ya mafuta yake kwisha. Pamoja na hayo , yumkini umri wa mtu ukafupika kwa sababu mbalimbali kama za kusibiwa na maradhi au ajali ya aina yoyote, sawa na taa ya kibatari ambayo pamoja na kuwa na mafuta lakini kwa sababu ya kuvumiwa na upepo, yumkini ikazimika. Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, mbali na kuchunga masuala ya vyakula na ya kiafya ambayo yanasaidia kurefusha umri wa mtu, kuna mambo mengine ambayo yametajwa kuwa hurefusha au kufupisha umri wa manaadamu. Kwa mfano kitendo cha kuunga udugu yaani Silatu-rahim, ambapo mwislamu anatakiwa kuwajali jamaa na ndugu zake, ni moja ya mambo yanayochangia kurefusha umri wa mtu. Pamoja na mambo mengine aya hii inatutaka tuelewe kuwa sisi hatukuja hapa duniani kwa irada na matashi yetu hata kuondoka kwetu nako kuwe mikononi mwetu. Hakuna ajuaye juu ya mwanzo au mwisho wa maisha yake hapa dunning; kama ni hivyo inakuwaje sisi tunakuwa wakanushaji wa wa chanzo cha ulimwengu huu na mwisho wake, yaani ulimwengu wa Akhera? Wa aidha tuelewe kwamba kuna mfumo maalumu unaotawala katika dunia hii tunayoishi, ambao ndio unaoainisha mwisho wa kila kiumbe. Mfumo ambao muumbaji na mtambuzi wake ni Allah (SW). Aya ya tatu ya sura hii inasema:
Na yeye ndiye Mwenyezi Mungu mbinguni na ardhini. Anajua ya ndani yenu na nje yenu, na anajua mnayoyachuma.
Baada ya aya mbili zilizotangulia kuzungumzia uwezo wa Allah wa kuumba mbingu na ardhi pamoja na mwanaadamu, aya hii inasema, basi tambueni kuwa kuna Mungu mmoja tu anayetawala mbingu na ardhi na Muumba wa kila kitu. Itikadi hii ni kinyume kabisa na mtazamo potofu wa wale wanaoamini kuwepo Mungu wa kila kitu., yaani mathalan mungu wa jua , mungu wa mvua, mungu wa mambo ya kheri, mola wa mambo ya shari n.k. Aya hii aidha inaashiria elimu isiyo na ukomo ya Allah ya kutambua matendo ya waja wake wanayoyafanya hadharani au wanayoyatenda kwa kificho, na kusema kwamba yeye Allah si Muumba wenu tu, bali pia ni mjuzi na mtambuzi wa hali zenu zote. Isikupitikieni kwamba yeye amekuumbeni tu na kisha akakuacheni kama mlivyo, sivyo hivyo asilani!. Yeye yuko karibu mno na nyinyi; anatambua kila mtendacho na kila mnachokiwaza ndani ya nafsi zenu. Kutokana na aya hii tunajelimisha kuwa, kama tuna imani ya yakini juu ya elimu ya Mwenyezi Mungu, basi bila shaka tutakuwa makini katika matendo na harakati zetu zote. Kwani hiyo itaweza kutuzuia kutenda vitendo viovu na itatutia raghba pia ya kutenda yaliyo mema. Tunajielimisha pia kwamba, kwetu sisi hali ya mbingu na ardhi na mambo ya siri na ya dhahiri ni vitu viwili tofauti kabisa, lakini kwa Mwenyezi Mungu Azza wa Jal, yote hayo yana hali moja katika elimu yake mutlaqi.

Porto v Arsenal VIP Trip - Premiership, Championship and all Football Betting Online - Paddy Power

Porto v Arsenal VIP Trip - Premiership, Championship and all Football Betting Online - Paddy Power

Kiongozi Muadhamu: Viongozi wa jamii wanapaswa kuweka wazi misimamo yao mbele ya adui

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya kiislamu ya Iran Ayatullah Ali Khamenei leo amehutubia hadhara kubwa ya maafisa wa Baraza la Uratibu la Jumuiya ya Ulinganiaji wa Kiislamu nchini na viongozi wa kamati za Alfajiri 10 na sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu akisema kuwa wadhifa wa wananchi wote hususan watu wenye nafasi za juu za kijamii katika kipindi cha fitina na mazingira ya kutatanisha ni kuonyesha msimamo wa wazi na kujiepusha na maneno na misimamo isiyoeleweka vyema. Ameongeza kuwa maadui daima wanapinga suala la kuwepo mazingira ya uwazi kwani wanaweza tu kufikia malengo yao katika mazingira ya kutatanisha na yenye fitina. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, katika kipindi cha sasa mirengo na makundi yote ya kisiasa ndani ya mfumo wa Kiislamu hapa nchini yanapaswa kuweka wazi misimamo na mipaka inayowatenganisha na maadui, na kwamba suala hilo ni wajibu zaidi kwa watu wenye ushawishi na taathira kubwa katika jamii. Si sahihi kuwa na msimamo au kutoa maneno yasiyokuwa ya wazi wakati viongozi wa ubeberu na dhulma na wavamizi wa nchi za Kiislamu wanapoingia katika medani na kudhihirisha misimamo yao. Ayatullah Khamenei amesema, wakati baadhi ya watu wanapokana Uislamu katika maneno na kupinga Jamhuri ya Kiislamu kivitendo kisha wakahoji uhalali wa uchaguzi wa Rais hapa nchini katika mazingira ya fitina na yaliyojaa vumbi, inatarajiwa kwamba watu wenye nafasi za juu katika jamii wanapaswa kudhihirisha wazi misimamo yao.Amesema: "uwazi ni adui wa maadui na kuzusha anga ya fitina na vumbi ni kumsaidia adui". Amesisitiza kuwa hicho ni kigezo na mizani ya utendaji kazi watu na makundi yote hususan tabaka la watu wenye nafasi za juu na ushawishi mkubwa katika jamii. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia njama mbalimbali zilizofanywa dhidi Mapinduzi ya Kiislamu katika kipindi cha miaka 30 iliyopita na akasema: "Taifa la Iran limepita katika misukosuko na vipindi vigumu mno kwa rehema yake Mwenyezi Mungu na litavuka mashaka kama hayo. Amesema kuwa maana ya mahudhurio hayo makubwa ya kila mwaka ni kuwa Mapinduzi ya Kiislamu na mfumo wake yanategemea wananchi na imani yao na hii ndiyo sababu kuu ya kushindwa kwa maadui katika njama zao za kuteteresha mfumo wa Kiislamu nchini Iran.Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa mti madhubuti wa Mapinduzi ya Kiislamu utaendelea kutoa matunda zaidi licha ya njama zote za maadui.