Wednesday, February 10, 2010

Mgosi: Wenger mnunue Rooney ili (kuiokoa arsenal).

MSHAMBULIAJI wa Simba, Mussa Hassan Mgosi amesema wataongeza nguvu maradufu kuanzia mechi ya leo Jumanne dhidi ya Manyema lakini akamshauri Arsene Wenger kuwa: "Tunamuhitaji Wayne Rooney wa Manchester United."

Mgosi, ambaye ni shabiki wa Arsenal aliyekerwa na vipigo viwili ilivyopata timu hiyo dhidi ya Manchester United mabao 3-0 na mabao 2-0 kutoka kwa Chelsea juzi Jumapili alidai kuwa wataifunga Liverpool kesho Jumatano.
"Kwa upande wa Simba tumejipanga vizuri sana na kuanzia mechi na Manyema tunaingia na nguvu mpya kabisa ambayo itakuwa ni zaidi ya mechi zilizopita," alisema Mgosi ambaye timu yake imepiga kambi kwenye hoteli ya Lamada jijini Dar es Salaam.

"Tumeamua kutumia nguvu zaidi kwavile tumegundua kwamba timu zimetupania sana kila tunapokanyaga ndio maana hata Kagera Sugar walipotoa sare na sisi wamefurahia sana, hivyo tumeamua kujidhatiti upya.

 "Hatutaki kuvuruga rekodi yetu na sidhani kama yaliyotokea Kagera yatajitokeza tena. Mashabiki wetu watupe sapoti na wasiwe na wasiwasi kwani tutafanya kazi."
Akizungumzia Arsenal, Mgosi alisema; "Arsenal tuko vizuri tunacheza mpira unaonekana kuanzia mwanzo, lakini tatizo hatuna mtu wa kutumbukiza kwenye nyavu."
"Mipira inakwenda vizuri kabisa tena kwa ufundi wa hali ya juu mpaka eneo la hatari, lakini hakuna wa kufunga, tunamhitaji mshambuliaji kama Jermain Defoe wa Tottenham au Wayne Rooney wa Manchester United, Kocha Arsene Wenger anahitaji kuliangalia hilo.
"Lakini ukiangalia pia kucheza mechi mfululizo na hizo timu kubwa nne ni tatizo, tumetoka Manchester hatujatulia tumekwenda kwa Chelsea sasa tunakwenda Liverpool hizo zote ni mechi ngumu sana na timu ikiteleza mechi moja ni rahisi sana kupoteza na inayofuata."

"Liverpool hawatuwezi, wale ni saizi yetu wanasuasua sana, hapa juzi juzi wamebahatisha tu kushinda lakini hawatufungi sisi Arsenal."
Lakini kocha wa Arsenal ni kama vile amemjibu Mgosi kwani jana Jumatatu aliiambia televisheni ya klabu hiyo kwamba; "Tulimiliki mpira vizuri sana lakini tulishindwa kuigeuza hali hiyo iwe ya ushindi wa mabao."

"Halafu wao wana uzoefu kuliko sisi, wale wana wastani wa miaka 29 sisi tuna kikosi cha wastani wa umri wa miaka 23. Ukicheza na hizi timu ukapoteza mchezo mmoja kisaikolojia ni madhara kwa mechi inayofuata, mechi ya Liverpool ni ngumu kama ilivyokuwa kwa Chelsea, lakini siwezi kukata tamaa tutapambana kama kawaida."