Wednesday, January 20, 2010

Suratul An'aam Aya ya 1 - 3

Sura hii iliteremshwa Makka na ina aya 165. Ujumbe mkuu wa sura hii ni kupamabana na shiriki na kulingania tauhidi kumpwekesha Mwenyezi Mungu); na hivyo nyingi kati ya aya zake zinabainisha itikadi za uzushi za Washirikina na Waabudu masanamu na kuweka wazi ubatilifu wa itikadi hizo. Aya za sura hii ya sita ya Quran Tukufu zinazungumzia pia masuala ya halali na haramu ya wanyama wa aina mbalimbali. Kwani kutokana na imani potofu walizokuwa nazo, Washirikina wa Kikureishi walijiharamishia baadhi ya wanyama ambao waliwaitakidi kwamba haijuzu kula nyama zao wala kuwatumia kama vipando. Ni kwa sababu ya kuzungumzia hukumu mbali mabali za wanyama wa miguu minne, ndiyo maana sura hii imepewa jina hili la al An-aam. Baada ya utangulizai huu mfupi, kwa pamoja sasa na tuitazame aya ya kwanza ya sura hii inayosema:
Sifa zote ni za Mwenyezi Mungu aliyeumba mbingu na ardhi na akafanya giza na mwangaza. Tena baada ya haya wale waliokufuru wamewafanya wengine sawa na Mola wao.
Aya hii tukufu inaanza kwa kumtambulisha Allah (sw) kwa waja wake na hasa wale wanaomshirikisha na pia wanaokanusha moja kwa moja kuwepo kwake. Aya inamtaja Mwenyezi Mungu kuwa ni yule aliyeumba mbingu na ardhi, hivyo kuwataka waeleze wale wanaoabudu asiyekuwa yeye, je hicho wanachokiabudu wao, kinao uwezo nacho wa kuumba? Aya inaendelea kusema , Mola huyo Allah, kwa kulipa nuru na mwangaza jua ameufanya ulimwengu yaani dunia hii ineemeke kwa mwangaza wenye joto unalohitajia, na kwa kuweka utaratibu maalum wa kuzunguka sayari mbali mbali, akalileta na giza kwa ajili ya mapumziko ya viumbe; sasa hao miungu wenu manowaabudu wanazo nguvu na uwezo wa kufanya kama hayo? Hapana shaka yeyote majibu ya masuali mawili hayo ni ‘hapana'. Kwa hivyo basi muelekeeni na kumuabudu Mola aliye mmoja na mweza wa kila kitu, na mhimidini na kumsifu Mola huyo kwa kuumba ulimwengu kama huu kwa ajili yenu. Aya hii inatoa maelezao ambayo yanavunja hoja za wanaoamini maada yaani Materialists amabo wanakana kabisa kuwepo muumbaji wa Ulimwengu huu, aidha inawarudi Washirikina yaani wanaoabudu Mungu zaidi ya mmoja, kama walivyo wafuasi wa dini ya Zartosht ambao itikadi yao ni kuwa mwangaza na giza ndiyo vyanzo vya ulimwengu. Kadhalika inavunja imani na itikadai potofu ya Washirikina wanaomuitakidi Allah kuwa ni Mungu aliye na mshirika. Kuna nukta moja yenye kutoa mguso wa kuvutia hapa, nayo ni namna Quran inavyoitaja nuru katika hali ya umoja tu, wakati neno giza daima linaonekana ndani ya kitabu hicho kitukufu katika sura ya wingi; hii ikimaanisha kwamba kwa kuwa nuru au mwangaza ni dhihirisho la uongofu, na kwa vile uongofu au haki ni moja tu, hivyo neno ‘muangaza' limekuja katika hali ya umoja. Lakini kwa vile njia za batili na upotofu ni nyingi, hivyo, kiza ambacho ni kielelezo chake kimekuja katika sura ya wingi. Kutokana na aya hii tunajielimisha kuwa Allah (sw) ndiye muumbaji wa kila kitu, na kwa hakika kuwepo au kutoweka kwa kila kitu kunafungamana na yeye. Tunajifunza pia kwamba, shirki ni aina mojawapo ya kufru. Kwani kukiitakidi kitu cho chote kile kuwa ni mshirika wa Allah, maana yake ni kukataa uwezo mutlaki wa Mola Muumba wa kukiendesha peke yake kila kitu cha ulimwengu huu.
Aya ya pili ya sura hii inasema:
Yeye ndiye aliyekuumbeni kwa udongo, kisha akakuwekeeni ajali, na muda maalumu uko kwake tu. Tena baada ya haya nyinyi mnafanya shaka.
Katika aya iliyopita , imezungumziwa kudura na uwezo mutlaqi wa Allah (sw) wa kuumba mbingu na ardhi. Katika aya hii linazungumziwa suala la kuumbwa mwanadamu kutokana na udongo usio na uhai, na kuhoji kuwa kama uhai na mauti yenu nyote yako mikononi mwa Mwenyezi Mungu, inakuwaje mnatilia shaka kuwepo kwake ? Katika aya hii zimetajwa ajali au nyakati mbili katika uhai wa mwanadamu , moja ikiwa ni muda wa ajali maalumu ambao anaujua Allah peke yake, na mwingine ni muda usio maalumu ambao unategemea mazingira ya kimaisha ya kia mtu. Kimsingi ni kwamba, Mwenyezi Mungu amemruzuku kila mtu uwezo na kipaji maalumu, uwezo ambao unapomalizika uhai wa mtu pia huisha, sawa na taa inayozimika baada ya mafuta yake kwisha. Pamoja na hayo , yumkini umri wa mtu ukafupika kwa sababu mbalimbali kama za kusibiwa na maradhi au ajali ya aina yoyote, sawa na taa ya kibatari ambayo pamoja na kuwa na mafuta lakini kwa sababu ya kuvumiwa na upepo, yumkini ikazimika. Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, mbali na kuchunga masuala ya vyakula na ya kiafya ambayo yanasaidia kurefusha umri wa mtu, kuna mambo mengine ambayo yametajwa kuwa hurefusha au kufupisha umri wa manaadamu. Kwa mfano kitendo cha kuunga udugu yaani Silatu-rahim, ambapo mwislamu anatakiwa kuwajali jamaa na ndugu zake, ni moja ya mambo yanayochangia kurefusha umri wa mtu. Pamoja na mambo mengine aya hii inatutaka tuelewe kuwa sisi hatukuja hapa duniani kwa irada na matashi yetu hata kuondoka kwetu nako kuwe mikononi mwetu. Hakuna ajuaye juu ya mwanzo au mwisho wa maisha yake hapa dunning; kama ni hivyo inakuwaje sisi tunakuwa wakanushaji wa wa chanzo cha ulimwengu huu na mwisho wake, yaani ulimwengu wa Akhera? Wa aidha tuelewe kwamba kuna mfumo maalumu unaotawala katika dunia hii tunayoishi, ambao ndio unaoainisha mwisho wa kila kiumbe. Mfumo ambao muumbaji na mtambuzi wake ni Allah (SW). Aya ya tatu ya sura hii inasema:
Na yeye ndiye Mwenyezi Mungu mbinguni na ardhini. Anajua ya ndani yenu na nje yenu, na anajua mnayoyachuma.
Baada ya aya mbili zilizotangulia kuzungumzia uwezo wa Allah wa kuumba mbingu na ardhi pamoja na mwanaadamu, aya hii inasema, basi tambueni kuwa kuna Mungu mmoja tu anayetawala mbingu na ardhi na Muumba wa kila kitu. Itikadi hii ni kinyume kabisa na mtazamo potofu wa wale wanaoamini kuwepo Mungu wa kila kitu., yaani mathalan mungu wa jua , mungu wa mvua, mungu wa mambo ya kheri, mola wa mambo ya shari n.k. Aya hii aidha inaashiria elimu isiyo na ukomo ya Allah ya kutambua matendo ya waja wake wanayoyafanya hadharani au wanayoyatenda kwa kificho, na kusema kwamba yeye Allah si Muumba wenu tu, bali pia ni mjuzi na mtambuzi wa hali zenu zote. Isikupitikieni kwamba yeye amekuumbeni tu na kisha akakuacheni kama mlivyo, sivyo hivyo asilani!. Yeye yuko karibu mno na nyinyi; anatambua kila mtendacho na kila mnachokiwaza ndani ya nafsi zenu. Kutokana na aya hii tunajelimisha kuwa, kama tuna imani ya yakini juu ya elimu ya Mwenyezi Mungu, basi bila shaka tutakuwa makini katika matendo na harakati zetu zote. Kwani hiyo itaweza kutuzuia kutenda vitendo viovu na itatutia raghba pia ya kutenda yaliyo mema. Tunajielimisha pia kwamba, kwetu sisi hali ya mbingu na ardhi na mambo ya siri na ya dhahiri ni vitu viwili tofauti kabisa, lakini kwa Mwenyezi Mungu Azza wa Jal, yote hayo yana hali moja katika elimu yake mutlaqi.

No comments:

Post a Comment