Thursday, January 21, 2010

MSIMAMO NGANGARI WA IRAN KUHUSIANA NA SUALA LA NYUKLIA.







Kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, nchi za Magharibi zilikuwa zikiishawishi Iran kujenga vituo na viwanda vya nyuklia kwa ajili ya kijidhaminia nishati ya umeme na matumizi mengineyo ya amani. Lakini mara tu baada ya ushindi wa mapinduzi hayo, nchi hizo na hasa Marekani, ziligeuka ghafla na kuanza kuiwekea vikwazo serikali ya Iran ili isiendelee mbele na mipango ya kukamilisha viwanda hivyo.
Jambo la kusikitisha ni kwamba, nchi za Magharibi zimekuwa zikiishinikiza Iran kisiasa na kiuchumi kwa lengo la kuizuia isinufaike na teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani na wakati huo huo kuimarisha ushirikiano wao kinyuklia na nchi kama vile utawala haramu wa Israel, Pakistan na India ambazo hazijatia saini mkataba wa NPT na ambazo zinatengeneza silaha hatari za nyuklia, tena nje kabisa ya usimamizi wa wakala wa IAEA. Siasa za kibaguzi za nchi za Magharibi zimezipelekea nchi hizo kuendelea kuibana Iran ambayo ni mwanachama wa IAEA na kutia saini mikataba muhimu ya kuzipa teknolojia ya kisasa ya nyuklia nchi hizo zilizotajwa, ambazo haziko tayari kutia saini mkataba wa NPT. Pamoja na kuwa nchi za Magharibi zinakiri wazi kwamba utawala wa kibaguzi wa Israel una zaidi ya vichwa 200 vya nyuklia na vile vile Korea Kaskazini kutangaza wazi kwamba imefanikiwa kurutubisha madini ya plutonium kufikia kiwango cha 90, lakini hakuna mashinikizo yoyote yanayotolewa wala hatua yoyote ya kisheria kuchukuliwa dhidi ya nchi hizo. Bali Iran ambayo imetia saini mkataba wa NPT, ndiyo inayokabiliwa na mashinikizo hayo ya kidhulma na kiuonevu. Kuhusiana na suala hilo, si tu kwamba nchi za Magharibi zilikwepa majukumu yao ya kisheria ya kukamilisha vituo viwili vya nyuklia vya Bushehr na Darkhoin ambavyo ujenzi wake ulikuwa umekamilika kwa asilimia 60 bali zimekuwa zikizuia na kuzishinikiza nchi nyingine zilizoamua kuvikalimisha vituo hivyo, ikiwemo Russia.


Undumakuwili unaofanywa na nchi za Magharibi kuhusiana na suala la nyuklia la Iran unadhihirisha wazi tabia ya kibaguzi ya nchi hizo. Katika hali ambayo tani 50 za gezi ya hexafloride ya urani ya Iran zimezuiwa nchini Ujerumani na pia asilimia kumi ya hisa za shirika la Ordif la urutubishaji urani huko nchini Ufaransa kumilikiwa na Iran, lakini Ufaransa na Uingereza zimekuwa zikivunja wazi sheria za kimataifa kwa kushirikiana kwa karibu na utawala ghasibu wa Israel katika uimarishaji wa silaha zake za nyuklia.
3- Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeonyesha nia yake yote njema katika kuthibitisha ukweli huu kwamba, mpango wake wa nyuklia ni wa malengo ya amani na kwamba unatekelezwa chini ya sheria na makubaliano ya kimataifa. Kabla ya mwaka 2004 na katika fremu ya mazungumzo ya ukosoaji yaliyofanyika kati yake na nchi za Ulaya, Iran ililiweka suala la nyuklia katika agenda ya mazungumzo hayo, ambapo baada ya majadiliano ya siku 9 ilifanikiwa kuweka wazi malengo yake kuhusiana na suala hilo. Katika kipindi hiki chote, IAEA imekuwa ikisimamia kikamilifu shughuli zake zote za nyuklia. Mbali na hayo, Iran ilichukua hatua ya kutazama na kutia upya saini mkataba wa NPT uliokuwa umemalizika muda wake nchini mwaka 1996. Licha ya hayo, ilichukua hatua ya kutia saini mikataba mingine muhimu ya kimataifa ikiwemo ya kuzuia majaribio ya silaha za nyuklia CTBT na kutoenezwa silaha za kemikali CWC. Hatua hizo zote zilichukuliwa na Jamhuri ya Kiislamuya Iran kwa madhumuni ya kuthibitisha nia yake kwamba, haina lengo la kutengeneza silaha za maangamizi ya umati. Pamoja na hayo, lakini nchi za Ulaya mwishoni mwa mwaka 2003 na mwanzoni mwa mwaka 2004, zilizidisha mashinikizo yao kwa ajili ya kuinyima Iran teknolojia ya nyuklia kwa tuhuma kwamba, Iran ilikuwa inakaribia kutengeneza silaha za nyuklia. Ili kuwathibitishia walimwengu kwamba ilikuwa ikitekeleza mpango wake wa nyuklia chini ya sheria na makubaliano ya kimatafa na pia kwa usimamizi na wakala husika wa masuala ya nyuklia, Iran ilichukua hatua zaidi, hata nje ya majukumu yake ya kisheria na inavyotakiwa na wakala wa IAEA, kwa shabaha ya kufikia lengo hilo.


Katika uwanja huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilifungua ukura mpya wa ushirikiano wa pande kadhaa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kwa kuchukua hatua zifuatazo:
1- Kutia saini kwa hiari, protokali ziada ya makubaliano ya kuzuia uenezaji wa silaha za nyuklia maarufu kwa jina la NPT. Hatua hiyo ilichukuliwa katika hali ambay, idadi kubwa ya nchi 81 wanachama wa wakala wa IAEA, bado hazijatia saini propokali hiyo. Hata Marekani yenyewe imekataa kupasisha na kutia saini protokali hiyo.
2- Kuonyesha ushirikiano mkubwa zaidi ya ule unaoainishwa na sheria za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.
3- Kuruhusu ukaguzi mkubwa, ambao haujawahi kushuhudiwa, wa wakala wa IAEA hapa nchini kwa maana kwamba, kwa wastani, wakaguzi zaidi ya wanne wa wakala huo wamekuwa wakikagua taasisi za nyuklia hapa nchini kwa siku.
4- Kuwasilisha ripoti yenye kurasa 1400 kuhusu shughuli na mipango yake ya nyuklia. Mbali na hayo, kumetolewa ripoti nyingine za maneno na katika mikutano mbalimbali kuhusiana na miradi ya nyuklia ya Iran.
5- Kuruhusu kufanyika mahojiano na mazungumzo na wataalamu wa nyuklia na baadhi ya wafanyakazi wa vituo vya nyuklia vya Iran.
6- Kuruhusu usimamizi na ukaguzi wa baadhi ya vituo vyake vya kijeshi.
7- Kusimamisha kwa muda shughuli zake za nishati ya nyuklia, utengenezaji wa vipuri, utafiti wa kinyuklia na kadhalika, kwa shabaha ya kujenga hali ya kuaminiana kimataifa.
Hatua hizo zimeonyesha kwamba, mipango ya nyuklia ya Iran haijakiuka sheria yoyote ya kimataifa, suala ambalo pia limeelezwa waziwazi na Katibu Mkuu wa Wakala wa IAEA katika ripoti zake nyingi.
Hata hivyo, Ulaya na Marekani si tu kwamba hazikujenga imani yoyote kuhusiana na hatua hizo za Iran, bali zimekuwa zikisisitiza juu ya matakwa yao yanayoitaka Iran itupilie mbali mpango wa kuwa na mfumo kamili wa kuzalisha mafuta ya nyuklia na kuendeleza siasa zao za uhasama dhidi yake.
4) Katika mtazamo wa Magharibi na hasa Marekani, iwapo teknolojia ya nyuklia ya Iran itaimarika na kupiga hatua za ustawi na maendeleo, hapana shaka kwamba nguvu ya kitaifa ya Iran kwa upande mmoja na uwezo wake wa kieneo na kimataifa katika upande mwingine, utakuwa na mabadiliko na atahari kubwa ulimwenguni. Mwenyekiti wa Taasisi ya Utafiti wa Kistratijia ya Ufaransa anasema, "sababu halisi ya juhudi za Marekani za kutaka kuizuia Iran isipate teknolojia ya nyuklia inafungamana na uwezo wa kistratijia wa Wairani. Uwezo huo wa kistratijia ni ile nafasi ya baadaye ya Iran kuwa nguvu kubwa zaidi katika eneo." Mtazamo huo pia umebainishwa na viongozi na wanastratijia wa Kimarekani katika misimamo na maandishi yao. Mmoja wao ni Izinshtain, ambaye ni afisa anayeshughulikia upangaji wa operesheni za kijasusi na kijeshi katika ofisi ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani. Izinshtain ameandika makala ndefu akisema, "wapo Iran itapata teknolojia ya nyuklia, suala la kuizuia Tehran isiutumie uwezo wake wa nyuklia kama satua na ushawishi wa kisiasa litakuwa changamoto kubwa kwa siasa za Marekani." Endelea < 1 2 3 >

Japokuwa sababu zinazowafanya Wamagharibi wapinge suala la Iran kuwa na teknolojia ya nyuklia ni zaidi ya hizo zilizotajwa, lakini Magharibi hususan Marekani inatumia uwezo na suhula zake zote kuinyima Iran haki yake ya wazi ya kuwa na miradi ya nishati ya nyuklia,
Nyenzo za kiuchumi ndicho chombo cha kwanza kabisa kinachotumiwa kukabiliana na Iran katika uwanja huo. Wapangaji wa siasa za mashinikizo dhidi ya Iran wanaona kuwa, kudhoofishwa kwa uchumi wa Iran kutaizuia nchi hii kuendeleza miradi mikubwa ukiwemo wa teknolojia ya nyuklia. Naibu Waziri wa Nishati wa Marekani, Bill White amesema kuhusiana na suala hilo kwamba: "Ninahamu ya kuona uchumi wa Iran ukidhoofika siku baada ya siku ili isiweze kutumia pato lake la fedha kujizatiti kwa silaha."
Vikwazo vya Marekani na Magharibi dhidi ya Iran vinajumuisha nyanja mbalimbali za teknolojia na hasa bidhaa zinazotumika kwa zaidi la lengo moja, vikwazo vya kifedha, uwekezaji, huduma na kadhalika.
Sera ya kuitenga Iran ni sehemu nyingine inayokamilisha siasa za Marekani na mataifa ya Ulaya za kuiwekea vikwazo serikali ya Tehran. Siasa hizo za kuidhibiti na kuibana Iran pia zinajumuisha utumiaji wa taasisi na mikataba ya kisheria kama vile mkataba wa protokali ziada ya makubaliano ya NPT, na kuishinikiza Iran ili iitie saini na kuipasisha, kubuni sheria zinazotolewa chini ya anuani ya ugaidi wa kinyuklia na kuziambatanisha na nchi kama vile Iran, kuuwekea mashinikizo Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na kuutaka ukate mashirikiano ya kiteknolojia na Iran na kadhalika. Hata hivyo, hatua hizo zisizokuwa za kisheria hazikuweza kuizuia Iran kufuatilia haki zake za kisheria.
Siasa za ulimwengu wa Magharibi za kusambaratisha na kuzuia ustawi wa sekta ya nyuklia ya Iran zilishika mwelekeo mpya tangu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipotangaza kwamba, imefanikiwa kupata teknolojia ya nyuklia. Hatua tau zilizingatiwa katika uwanja huo. Kusitisha kwa muda, kusimamisha na hatimaye kuharibu kabisa taasisi za nyuklia za Iran. Ili kukamilisha lengo hilo, Wamagharibi waliingia katika vita tata dhidi ya Iran, huku Marekani ikichukua nafasi ya polisi mbaya nayo Ulaya kuvaa joho la msamaria mwema. Katika hali hiyo, Marekani ililizingatia suala la kupelekwa faili la Iran katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa lengo lake la kistratejia, ilhali Ulaya ilichagua stratejia ya hatua kwa hatua.
Mwanzoni mwa mwaka 2005, Wamagharibi walidhani kwamba wameweza kutekeleza hatua ya kwanza na ya pili ya mpango wao. Kwa msingi huo, miezi kadhaa baadaye, walifanya kikao cha kistratijia na kutangaza kuwa njia pekee ya kutoa dhamana kwamba miradi ya nyuklia ya Iran inafanyika kwa malengo ya amani ni Tehran kutupilia mbali mpango wake wa kuwa na mfumo kamili wa kuzalisha mafuta ya nyuklia. Muda mfupi baadaye, nchi hizo ziliwasilisha pendekezo hilo kwa Iran kimaandishi na zikaitaka tena kufutilia mbali shughuli zake za nyuklia.
5) Baada ya kubainika wazi malengo halisi ya watu wa Ulaya kuhusiana na shughuli za nishati ya nyuklia za Iran, na Tehran kukata tamaa kuhusiana na uwezekano wa kupata haki zake za nyuklia kupitia mwenendo wa mazungumzo na Ulaya, na pia kwa kutilia maanani matokeo ya uchaguzi wa tisa wa rais nchini, udiplomasia wa nyuklia wa Iran ulishuhudia mabadiliko maalumu. Kwani kwa hakika kudumishwa kwa mwenendo wa huko nyuma na njama za kutaka kusimamishwa kwa shughuli zote za nyuklia za Iran hazikuwa na hatima nyingine ghairi ya Iran kunyimwa haki yake ya kisheria ya kunufaka kwa amani na teknolojia ya nyuklia. Kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilibadili kanuni za mchezo na kwanza ikachukua hatua ya kufungua tena kiwanda chake cha UCF huko Isfahan. Baadaye ilianzisha tena shughuli za utafiti wa nyuklia uliokuwa umesimamishwa kwa muda, na katika hatua ya tatu ikasimamisha utekelezaji wa hiari wa protokali ziada ya mkataba wa NPT na kisha shughuli nyingine za nyuklia zikaanza tena kufuatia amri iliyotolewa na Rais Mahmoud Ahmadinejad. Kufuatia hatua hiyo ya Iran, nchi za Ulaya zilisimamisha mazungumzo yao na Tehran. Badala yake zikaandaa kikao cha dharura cha Bodi ya Magavana na kupitisha maazimio yenye maneno makali dhidi ya Iran. Hata hivyo, kusimama kidete Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mbele ya mashinikizo ya Magharibi, yalizifanya nchi hizo za Ulaya zilazimike kukubaliana na baadhi ya matakwa ya Iran. Baada ya kudhihirikiwa na jinsi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilivyosimama kiume kutetea haki yake na kuonyesha kuwa haitishiki na suala la faili lake la nyuklia kupelekwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, nchi za Ulaya zilijikuta zikilazimika kuikubali haki ya Iran kuhusiana na taasisi yake ya UCF ya ubadilishaji urani iliyoko Isafahan, na uzalishaji wa gesi ya Hexafloride. Hata hivyo, nchi hizo zilishurutisha urutubishaji wa urani ufanyikie katika ardhi ya nchi nyengine. Hilo kwa hakika ndilo pendekezo kuu lililokuwemo katika mpango uliopendekezwa na Russia. Kuanzia hapo na kuendelea, ujanja na mashinikizo ya nchi za Ulaya yalilenga katika kuifanya Iran ikubaliane na mpango huo. Hata hivyo, Iran ambayo tokea hapo awali ilikuwa imeshasisitiza kwamba suala la kujizalishia yenyewe mafuta ya nyuklia ni mstari mwekundu usioweza kuvukwa na pia ni sehemu ya maslahi yake ya kitaifa, iliukataa mpango huo na kutangaza kuwa mpango huo unaweza kukubalika iwapo tu utachukuliwa kuwa ni sehemu ya ukamilishaji mradi wa urutubishaji urani ndani ya ardhi ya Iran. Radiamali hiyo ya Iran iliyafanya madola ya Magharibi yazidishe mashinikizo yao, yaliyofikia kilele chake kwa kuitisha kikao cha dharura cha Bodi ya Magavana ya IAEA na kupasisha azimio la kuliripoti faili la nyuklia la Iran kwenye Baraza la Usalama.
Hakuna shaka kuwa si kwa kupitia Baraza la Usalama wala kwa kutumia njia nyingine yoyote, nchi za Magharibi hazina uwezo wa kuifanya Iran iachane na haki yake halali na ya kisheria ya kujipatia teknolojia ya nyuklia. Wapanga mikakati na wanafikra wa serikali za magharibi wanakubaliana kwa kauli moja kuwa, hatua za kijeshi, vikwazo vya kiuchumi na kulipeleka faili la nyuklia kwenye Baraza la Usalama hakutowezesha kupatikana ufumbuzi wa suala la nyuklia la Iran. Kwa mtazamo wa wataalamu hao, uwezo wake wa kijeshi, idadi yake ya watu, ubora wa nguvu kazi yake, nafasi yake ya kipekee ya kijografia katika eneo la Mashariki ya Kati, mshikamano ulioko ndani ya nchi kati ya wananchi na serikali yao pamoja na uwezo na ushawishi wa Kiongozi Mkuu kwa wananchi, yote hayo yameifanya serikali ya Iran kuwa na uimara wa kiwango ambacho inakuwa ni njozi kwa mtu kufikiria suala la kuiangusha serikali hiyo kupitia uvamizi wa kijeshi. Wataalamu na wanafikra hao wa Magharibi aidha wanaamini kwamba, endapo kutachukuliwa hatua za kijeshi au za uwekaji vikwazo dhidi ya Iran, matokeo ya uchukuaji hatua hizo yatakuwa mabaya mno. Na ndiyo maana si wataalamu hao tu bali hata viongozi wengi wa nchi za Ulaya wamekuwa wakitahadharisha mara kwa mara juu ya uchukuaji hatua yoyote ya kijeshi au kuiwekea vikwazo Iran. Hata hivyo, baada ya kuthibitikiwa na uhakika huo, wa kwamba si mashinikizo ya kisiasa wala vitisho vya kijeshi na vya vikwazo vya kiuchumi vinavyoweza kuifanya Iran ilegeze kamba katika mpango wake wa nyuklia, wanafikra na wapanga mikakati wa sera za madola ya Magharibi wamefikia natija kuwa, vita vya kinafsi na kisaikolojia ndiyo njia bora ya kukabiliana na Iran, kwa kuzingatia kuwa kujiamini kwa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kutoyumba katika msimamo wake juu ya mpango wake wa nyuklia, kwa kiwango kikubwa kumetokana na uungaji mkono mkubwa wa wananchi ambao wanalichukulia suala hilo la nyuklia kuwa fakhari yao ya kitaifa. Hivi sasa tunashuhudia wazi wazi utekelezaji huo wa vita vya kinafsi na kisaikolojia vya Magharibi hasa kutoka kwa Marekani dhidi ya Iran. Kwa upande wake, kituo cha kistratejia cha Heritage kimeishauri serikali ya Washington juu ya utekelezaji wa operesheni hiyo ya vita vya kinafsi kuwa, ili kuiusambaratisha ungangari wa Iran, ni lazima hujuma za vita hivyo zielekezwe kwa watu ndani ya nchi hususan tabaka la vijana. Katika stratejia na mkakati mpya wa Magharibi hasa Marekani, wa kufanikisha kile kinachoitwa "mpango wa kuufunga mradi wa nyuklia wa Iran", kuna malengo matatu yanayofatiliwa kwa wakati mmoja. La kwanza ni kujaribu kuwatia khofu wananchi kuwa watafikwa na matokeo mabaya kutokana na siasa za serikali ya Iran ya kutokuwa tayari kuachana na mpango wake wa nyuklia, sambamba na kujaribu kuonyesha kuwa kutaka kujipatia teknolojia ya nyuklia ni suala lisilokuwa na faida kwa Iran. Lengo la pili, ni kujaribu kuleta mgawanyiko kati ya serikali na wananchi, na tatu ni kuidhoofisha serikali ya Jamhuri ya Kiislamu.
Ni kwa kuzingatia hali hiyo ndipo ikahisika wazi kuwa, hivi sasa kuna umuhimu mkubwa zaidi kwa wananchi kuyalinda matunda na mafanikio ya nyuklia iliyoyapata Iran kama walivyofanya wananchi hao huko nyuma kwa mfumo wao wa Kiislamu. Hakuna shaka kuwa haki si ya kupewa bali ni kitu cha kuchukua, hivyo basi ili kuweza kujichukulia haki yake halali ya nyuklia, taifa la Iran linapaswa kuwa na istiqama na kusimama kidete juu ya suala hilo. Kulingana na mafundisho matukufu ya Uislamu, kuwa na irada na azma thabiti, pamoja na imani ya kweli kwa lengo na njia ambayo taifa la Kiislamu limejichagulia, hulipa ushindi taifa hilo katika mapambano ya kufikia lengo lake hata kama Waislamu watakuwa wachache kiidadi. Mwisho

No comments:

Post a Comment